Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kutoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini unapimwa kwa kipimo cha mwezi.
Na. Aron Msigwa - Dar es salaam
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Machi umeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Machi 2014 umeongezeka na kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.0 mwezi uliopita.
Amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2014 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Februari huku kukiwa na ongezeko dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma mwezi huu ikilinganishwa na bei za mwezi Machi mwaka jana.
Ameeleza kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Machi umeongezeka hadi asilimia 7.9 kutoka asilimia 6.9 za mwezi Februari mwaka huu huku badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 5.2 kwa mwezi Machi 2014 kutoka asilimia 6.2 za mwezi Februari.
Amefafanua kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga, ulezi na matunda, ndizi za kupika na maharage zimeonyesha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mwezi Machi ikilinganishwa na bei za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei za bidhaa zisizo za vyakula za vitambaa vya suti za wanaume, gharama ya usafi wa nywele na usafi binafsi, Petroli, mkaa, huduma za matibabu pamoja na tiketi za kutazama mpira wa miguu ligi kuu zikionyesha ongezeko.
Kwa upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko dogo kwa asilimia 0.6 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.4 kwa mwezi Februari mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 149.49 kwa mwezi Machi kutoka 140.93 za mwezi Machi mwaka uliopita huku fahirisi za zinazopimwa kwa kipimo cha mwezi zikifikia asilimia 149.49 kutoka 148.62 za mwezi uliopita.
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na nyanya, viazi vitamu, matunda, mchele, tambi na kuku wa kisasa ambao wameongezeka kwa asilimia 1.8.
Aidha kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Machi umepungua na kufikia shilingi 66 na senti 90.
“Kupungua kwa thamani ya Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa Shilingi 100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua kitu kama kile kile, kwa mfano badala ya shilingi 100 inabidi atumie shilingi 134”
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umepungua kidogo na kufikia asilimia 6.27 kwa mwezi Machi kutoka asilimia 6.86 za mwezi Februari , huku Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 7.1 kwa mwezi Machi ikilinganishwa na asilimia 6.8 za mwezi uliopita.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment